12.08.2015

wahitimu chuoni mzumbe wahimizwa ktumia elimu zao vyema
 
WAHITIMU Chuo Kikuu Mzumbe wameshauriwa kutumia elimu waliyoipata katika kuchochea maendeleo ya chuo hicho na ya taifa kwa ujumla. Rais wa Masajili ya chuo hicho, (Mzumbe University Convocation), Ludovick Utouh ambaye pia ni Mkaguzi Mkuu mstaafu wa Hesabu za Serikali, alitoa mwito huo katika mkutano wa masajili ya 15 ya chuo mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.
“Wote tuliosoma hapa na tukapata muongozo mzuri wa elimu na kufikia nafasi tulizonazo mahali popote tulipo, tujione tuna wajibu wa kushiriki kukisaidia chuo chetu,” alisema Utouh.
Awali, kabla ya kuwa Chuo Kikuu, kilijulikana kama Chuo cha Maendeleo Mzumbe (IDM).
Alisema michango inayohitajika kutoka kwa wahitimu hao ni pamoja na mawazo yao ya kitaaluma katika kuboresha mitaala, kuboresha miundombinu, kubadilishana uzoefu na mawazo.
Akitoa mfano alisema wale wote ambao wamekuwa wakishiriki katika kukisaidia wamefanikisha kujenga Bweni la Mama Maria Nyerere kwa ajili ya wanawake na kutatua changamoto mbalimbali chuoni hapo.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Josephat Itika alisema wamepanga Juni 24 mwakani kufanya mkutano utakaowakutanisha wahitimu wote waweze kutoa michango yao na kubadilishana mawazo na uzoefu kwa maendeleo ya chuo.
Aliwataka wahitimu hao ambao hawajajiorodhesha katika masajili ya chuo kufanya hivyo kupitia tovuti ya chuo ya www.mzumbe.ac.tz ili kurahisisha mawasiliano na wenzao.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Profesa Daniel Mkude alitoa zawadi kwa wahadhiri waliochapisha machapisho mbalimbali na kuwataka kuendelea kufanyakazi hiyo na kuzidi kuboresha maudhui.
“Hii ni taasisi ya elimu ya juu na wahadhiri pamoja na kazi ya kufundisha pia mna wajibu wa kufanya tafiti na kuandika machapisho mbalimbali,” alisema.
Sambamba na hilo pia alitoa zawadi mbalimbali ikiwemo vyeti kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao na kuwataka kuongeza bidii katika kutafuta maarifa zaidi nje ya taaluma zao.

No comments:

MAELEKEZO YA KUJIUNGA NA SEKONDARI KIDATO CHA TANO

UPDATES:HIZI HAPA JOINING INSTRUCTIONS ZOTE ZA FORM V/KIDATO CHA TANO(5) 2017/2018   MAELEKEZO YA KUJIUNGA NA SEKONDARI...